Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza Arafi, Mkurugenzi wa Hawza nchini Iran, ambaye amezuru Bosnia na Herzegovina kwa ajili ya kushiriki katika hafla ya Hati ya Uongozi Rais mpya wa Jumuiya ya Kiislamu ya Bosnia na Herzegovina, amezungumzia masuala mbalimbali ya sasa katika mahojiano aliyofanya na tovuti ya habari ya Klix.ba.
Katika mahojiano hayo, alizungumzia mzozo na mapigano yanayoendelea kati ya Iran kwa upande mmoja na Israel pamoja na Marekani kwa upande mwingine. Pia alizungumzia uhusiano kati ya Iran na Bosnia na Herzegovina, pamoja na nafasi na mchango wa nchi hizo mbili katika nyanja za utamaduni na sanaa.
Yafuatayo ni maudhui ya mahojiano hayo:
Swali: Baada ya kuuawa kishahidi Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, ulikuwa miongoni mwa wajumbe wa Baraza la Muda la Uongozi. Mchakato wa kufanya maamuzi katika vikao vya baraza hilo ulikuwaje, na ni suala gani lililokuwa gumu zaidi mlilokabiliana nalo katika kipindi hicho?
Ayatullah Arafi: Baada ya kuuawa kishahidi Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, tulikabiliana na uzoefu mpya katika kipindi cha baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu; uzoefu ambao ulikuwa tofauti kabisa na uzoefu wetu wote wa hapo awali. Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi aliuawa kishahidi, na makamanda kadhaa pia waliuawa katika mashambulizi yaliyolengwa dhidi yao. Kutokana na hali hiyo, baadhi ya nguzo za mfumo wa utawala wa nchi zilidhoofishwa.
Wakati huohuo, jambo lililotuvutia na tulilolipa umuhimu mkubwa lilikuwa mwitikio wa wananchi na raia wa kawaida, ambao mara moja walijitokeza mitaani kuunga mkono mfumo wa utawala wa nchi yao na kulinda taifa lao.
Jambo jingine ni kwamba Kiongozi wetu aliyeuawa kishahidi alikuwa amefanya maandalizi muhimu kabla ya kuuawa kwake, kwa ajili ya kuhakikisha mwendelezo wa mamlaka na uendeshaji wa shughuli za nchi. Hili lilikuwa jambo muhimu sana. Aidha, alikuwa amebainisha njia ya kuendeleza harakati ya Muqawama.
Mambo haya matatu kwa pamoja yalisaidia kuzuia nchi yetu kusambaratika. Hili ni jambo ambalo tunapaswa kulisisitiza.
Kuhusu Baraza la Muda la Uongozi, napenda kusema kwamba baraza hilo liliundwa mara moja baada ya kuuawa kishahidi, au kwa usahihi zaidi, kuuawa kwa Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi. Katika kipindi cha siku hizo chache, lilifanya maamuzi mbalimbali kuhusu uendeshaji wa shughuli za nchi.
Swali: Je, unaunga mkono mazungumzo na Washington? Je, njia hiyo inaweza kusababisha kuimarika utulivu katika Mashariki ya Kati?
Ayatullah Arafi: Iran daima imekuwa ikishikamana na mazungumzo na majadiliano. Jambo alilolifanya Donald Trump, ambalo huenda ni baya hata kuliko vita vyenyewe, ni kuharibu hadhi na uaminifu wa mazungumzo katika ngazi ya kimataifa. Hii ni kwa sababu katika mara mbili tofauti, tulipokuwa katika hatua za kufanya mazungumzo, aliishambulia nchi yetu. Kwa hiyo, kwa vitendo vyake hivyo, amedhoofisha na kuharibu hadhi pamoja na uaminifu wa mazungumzo katika ngazi ya kimataifa.
Kwa sababu hiyo, Iran haijawahi kukataa mazungumzo na majadiliano. Hata hivyo, daima imesisitiza umuhimu wa kulinda na kuheshimu haki za wananchi. Iran, iwe wakati wa mapigano au baada ya mapigano, imeendelea kusisitiza utayari wake wa kuendeleza Muqawama na kusimama imara kwa lengo la kutetea haki za taifa la Iran.
Wale walioishambulia nchi yetu walitenda jinai mbalimbali, zikiwemo jinai dhidi ya ubinadamu. Kwa mfano, katika siku za mwanzo za vita, walishambulia shule moja na kuwaua kishahidi wanafunzi wengi katika shambulio moja pekee. Hiyo ni mojawapo tu ya mifano ya uhalifu huo.
Mbali na hayo, waliitaka rasmi nchi yetu isalimu amri na kuinamisha kichwa. Pia walitishia waziwazi kwamba wangeangamiza ustaarabu wenye historia ya maelfu ya miaka. Kwa maneno mengine, kupitia vitisho hivyo, walivuka mipaka yote ya utu na ubinadamu.
Kuna jambo jingine muhimu hapa, nalo ni kwamba shambulio hilo halikulenga Iran pekee, bali athari na madhara yake yalienea hadi maeneo mengine ya dunia. Hali ilifikia hatua ambapo hata nchi za Ulaya zilikumbana katika maeneo yao na athari za hatua hizo pamoja na vita vilivyolazimishwa dhidi ya Iran.
Sisi hatukuwa waanzilishi wa vita. Hata hivyo, linapokuja suala la kujilinda na kulinda haki za taifa letu, hatutambui mpaka wowote mwekundu, na tuko tayari kutumia uwezo wetu wote katika kutetea haki hizo.
Inatarajiwa kwamba Ulaya haitafuata nyayo za Marekani na utawala wa Kizayuni katika hatua zao.
Swali: Je, hii ndiyo ziara yako ya kwanza nchini Bosnia na Herzegovina? Iran ya leo ina mtazamo gani kuhusu Bosnia na Herzegovina pamoja na Waislamu wa eneo la Balkan? Ungependa kujenga uhusiano wa aina gani na nchi kama yetu?
Ayatullah Arafi: Katika miaka michache iliyopita, nimetembelea eneo la Balkan na nchi yenu mara moja au mbili. Uhusiano wetu na eneo hili una mambo mengi yanayofanana na yanayotukutanisha, ambayo yanaonekana zaidi katika nyanja ya utamaduni.
Ziara yangu ya sasa nchini Bosnia na Herzegovina imefanyika kwa mwaliko wa Jumuiya ya Kiislamu ya nchi hii, kwa lengo la kushiriki katika hafla ya kukabidhi Mamlaka kwa Rais mpya wa Jumuiya ya Kiislamu ya Bosnia na Herzegovina. Tunatumaini kwamba ziara hii pia itachangia katika kuendeleza uhusiano kati ya nchi hizi mbili, hususan katika nyanja za utamaduni, fikra na mawazo, pamoja na sanaa.
Napenda kusisitiza tena kwamba Iran inajitahidi kuimarisha na kupanua uhusiano wake na nchi zote za eneo lenu, na kwa maana hiyo, na mataifa yote yanayoishi katika nchi yenu. Tunatumaini kwamba katika siku zijazo tutashuhudia uhusiano ulio bora zaidi na wenye nguvu zaidi.
Ziara hii pia imebeba ujumbe kwamba nchi yetu, kama ilivyokuwa hapo awali, bado iko tayari kuimarisha, kupanua na kuboresha uhusiano wake na nchi yenu katika nyanja zote.
Swali: Vita vya Bosnia na Herzegovina na mauaji ya kimbari ya Srebrenica vinakumbukwaje nchini Iran, hususan miongoni mwa wanazuoni wa dini? Je, masuala haya yanafundishwa katika madrasa za elimu ya dini na Hawza?
Ayatullah Arafi: Iran, kwa mtazamo wa kibinadamu na wa Kiislamu, inapoona dhuluma na jinai zikifanyika dhidi ya binadamu katika sehemu yoyote ya dunia, hujiona kuwa na wajibu wa kuwasaidia watu wenye mahitaji na wanaodhulumiwa kwa kadiri ya uwezo wake. Mtazamo huu umekuwepo daima. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, hali hiyo ilionekana kwanza nchini Afghanistan, kisha Gaza na katika maeneo mengine. Kwa hiyo, Iran daima imekuwa ikichukulia kuwasaidia wahitaji na wanaodhulumiwa kuwa ni wajibu wa kidini.
Bado tuna mapenzi na hisia za pekee kwa Bosnia na Herzegovina pamoja na wananchi wake. Kama nilivyotangulia kueleza, tunataka kuendeleza na kuimarisha uhusiano wetu na nchi yenu.
Swali: Lugha na ushairi wa Kifarsi, kuanzia kwa Mawlana hadi Hafez, vimekuwepo nchini Bosnia kwa karne nyingi, na miswada mingi ya kazi za Kifarsi inahifadhiwa katika maktaba za Sarajevo. Ni mambo gani yanayoziunganisha Iran na Bosnia na Herzegovina katika zama hizi?
Ayatullah Arafi: Mbali na uga wa fasihi, hususan katika nyanja ya ushairi, lugha na mijadala inayohusu vipengele vya kiroho vya eneo hili, ninaamini kwamba tunaweza pia kuweka na kuendeleza misingi ya ushirikiano katika uga wa falsafa.
Zaidi ya hayo, kuna uga mwingine muhimu, nao ni fasihi, hususan fasihi ya Muqawama. Hii ni kwa sababu ninyi pia mmepitia kipindi cha Muqawama, nasi pia tumepitia uzoefu huo. Kwa hiyo, ninaamini kwamba tunaweza kuweka misingi ya ushirikiano wa pamoja katika eneo hili pia.
Kwa upande mwingine, balozi wetu aliyepo hapa yuko tayari kikamilifu kuendeleza uhusiano na ushirikiano katika nyanja zote hizi. Nasi pia, kupitia taasisi na vituo vya elimu vilivyopo nchini Iran, tunatangaza utayari wetu wa kupanua ushirikiano huo.
Zingatia:
Klix.ba: Jina la tovuti ya habari ya Bosnia
Maoni yako